CHAMA cha Tanzania Labour(TLP) kimemuandikia barua Rais wa Mapinduzi wa
Zanzibar, Dk Mohamed Ali Shein na kumtaka kuanzia sasa wamtenge Katibu
Mkuu wa CUF , Maalim Seif Sharif Hamad (pichani), kwa kutomualika kwenye
shughuli zozote za kitaifa mpaka atakapojirekebisha na kuitambua rasmi
serikali iliyopo madarakani.
Aidha, kwa kuwa CUF inadai kwamba haiitambui serikali hiyo basi ruzuku
kwa chama hicho isitishwe kuanzia sasa hadi hapo chama hicho
kitakapoitambua rasmi serikali hiyo na kuacha kuhamasisha wananchi
wasilipe kodi.
Katika barua ya chama hicho iliyosainiwa na Mwenyekiti wake, Augustine
Mrema ilisema chama hicho kimesikitishwa na wanalaani kitendo
kilichofanywa Hamad ambaye pia alikuwa Makamu wa kwanza wa Rais kwenye
serikali ya Umoja wa kitaifa wa Zanzibar (SUK) wakati wa maziko ya
aliyekuwa Makamu wa Rais wa serikali ya Muungano wa Tanzania na Rais wa
Zanzibar, marehemu Mzee Aboud Jumbe cha kukataa kumpa Rais Shein mkono
wa kusalimiana.
Alisema kuleta tofauti za kisiasa msibani kwa makusudi, Maalim Seif
ameendelea kuwagawa Wazanzibari kisiasa na kushindwa kumuenzi marehemu
Aboud Jumbe, ambaye pamoja na kuiongoza Zanzibar kwa amani na utulivu
pia ndiye aliyemlea Maalim Seif kisiasa.
Alisema tangu kumalizika kwa uchaguzi mkuu wa marudio uliosusiwa na CUF,
Maalim Seif amekuwa akileta chokochoko na uchochezi dhidi ya serikali
ya Zanzibar akidai kwamba haitambui na kuwataka wananchi wa Zanzibar
kugoma na kuwataka wasilipe kodi kwa serikali
Tagged with: SIASA
Hakuna maoni :