SALVATORY EDWARD |
Kiungo
wa zamani wa timu ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo
(DRC), Ngawina Ngawina, pamoja na kiungo wa zamani wa Yanga, Salvatory
Edward wameanzisha kituo cha kuibua vipaji vya wanasoka chipukizi chini
ya umri wa miaka 17 na kuviendeleza.
Akizungumza
Dar es Salaam jana, Ngawina alisema kituo chao kinaitwa Kambiasso
Sports na kwamba kwa kuanzia Jumamosi wiki hii watafanya kliniki maalum
ya kusaka vipaji hivyo kwenye Uwanja wa Tandika Mabatini, Dar es Salaam,
dhamira yao kubwa ikiwa ni kuhakikisha wachezaji wenye vipaji
wanaendelezwa na kutafutiwa timu.
“Kila
mzazi mwenye mtoto ambaye anaamini ana kipaji cha soka na anahitaji
aendelezwe, amlete mwanae Tandika Mabatini Jumamosi Agosti 27, ajitahidi
saa mbili asubuhi awe ameshafika, kwani ndiyo muda tutakaoanza.
“Kliniki
yetu itaendeshwa na makocha mahiri, ambao wana leseni za ukocha kutoka
Caf (Shirikisho la Soka Afrika), ili kufanya hili jambo kiuweledi zaidi
na kupata vijana wenye sifa,” alisema Ngawina.
Alisema
dhamira yao ni kupata vijana wengi wenye vipaji kadri iwezekanavyo na
kwamba suala la idadi itategemea na watakavyoona siku hiyo, lakini
dhamira yao ni kuwa na vijana wasiopungua 30, lakini si lazima wote
wapatikane Dar es Salaam, wataenda hadi mikoani.
Aliwataja
watakaoendesha mshujo huo licha ya yeye na Salvatory, pia atakuwepo
kocha Kennedy Mwaisabula, ambaye amepata kufundisha timu mbalimbali
nchini ikiwemo Yanga.
Mwingine
ni kipa wa zamani wa timu mbalimbali ikiwemo Simba ya Dar es Salaam na
Ferroviario De Maputo ya Msumbiji, Muharami Mohammed ‘Shilton’, ambaye
kwa sasa ni kocha wa makipa wa timu ya Taifa ya vijana chini ya umri wa
miaka 17 ‘Serengeti Boys’ . Pia atakuwepo kocha mwingine wa makipa Terry
Muhorel.
“Soka si kama paa la nyumba kwamba siku zote linakuwa juu tu. Soka inaanzia chini na ndiko tunakotaka twende,” alisema Ngawina.
Kwa
upande wake Salvatory alisema dhamira yao ni kuwa na kituo ambacho
kitakuwa hazina ya nchi kwa wachezaji wa siku za usoni, lakini pia kiwe
kitovu cha timu mbalimbali kuchukua wachezaji.
“Tunaamini
vijana wetu wakishaiva tutawauza timu mbalimbali za ndani ya Tanzania
na nje, kwani kituo kina uhusiano mzuri na watu mbalimbali waliopo hapa
nchini na hata nje ya nchi,” alisema Salvatory.
“Tunaosimamia
jambo hili tumecheza mpira kwa kiasi cha kutosha, tumesomea ukocha,
tunajua nini cha kufanya kuendeleza vijana wetu,” alisema.
Aliwaomba
wachezaji chipukizi wa umri huo wanaoamini wana uwezo wajitokeze siku
hiyo ili kuwania nafasi ya kuwepo katika kituo hicho ambacho kitakuwa
Temeke, Dar es Salaam.
Hakuna maoni :