Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, amesema wamegundua njama za kuiba
kura zitakazofanywa na CCM usiku wa tarehe 24 kwa kupita mitaani na
kugawa fedha za kura feki.
Mbowe alitoa kauli hiyo jana kwenye mkutano wa kampeni uliofanyika katika Viwanja vya Ruanda Nzovwe vilivyopo jijini Mbeya.
Alisema ili kudhibiti hali hiyo, siku hiyo Ukawa watafanya doria usiku
kucha ili kuhakikisha hakuna fedha zinazogawiwa wala kura feki
zitakazosambazwa.
“Nia ya Ukawa ya kupigania Katiba ya wananchi iko pale pale kwani
Serikali ya awamu ya tano itaipigania kadri itakavyowezekana ili kiu ya
wananchi juu ya Katiba hiyo ipatikane,” alisema Mbowe.
Alisema pia kwamba, uchaguzi wa mwaka huu ni wa kihistoria kwa kuwa
unahusu maisha ya watu, watoto na utajibu maombi ya Watanzania.
Pamoja na hayo, alisema Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), siyo huru na
kwamba wanachama wa Chadema watahakikisha wanalinda kura zao.
“Kwa miaka 25 tumepiga kelele tukidai tume huru ya uchaguzi lakini
kilio chetu hakikusikika kwa sababu CCM inajua tukiwa na tume huru,
haiwezi kubaki madarakani.
“Kama tume yetu siyo huru, tuna wajibu wa ziada wa kulinda kura zetu.
sheria inasema huturuhusiwi kusimama wala kukaa chini ya mita 200
kutoka kituoni. Kwa hiyo, ukihesabu mita 200 kutoka kituoni, una uhuru
wa kuwa eneo hilo,
“Jambo hili limezua hofu ndani ya tume, ndani ya Serikali, ndani ya
CCM na kwa Rais Jakaya Kikwete kwa sababu anasema tukishapiga kura,
tukalale. Sasa namwambia Rais Kikwete ushauri huo akawape CCM, sisi
hatuutaki,” alisema Mbowe.
Alisema pia kwamba, wanachama wa Chadema na wapenzi wao, hawatafanya
fujo bali watakuwa na ujasiri wa kupiga na kulinda kura zao kwa sababu
hakuna anayeweza kuzuia mpango wa Mungu kwa kutumia askari au nguvu.
Source:Mpekuzi blog
Tagged with: SIASA
Hakuna maoni :