WAKATI Rais John Pombe Magufuli akitegemewa kutangaza Baraza la Mawaziri
wakati wowote kuanzia sasa, matumbo ya wabunge yamepata moto
wakijiuliza kama watawezana na kasi yake endapo watateuliwa kuwemo.
Magufuli, ambaye Rais Mstaafu Jakaya Kikwete alimuita Tingatinga,
ameweka wazi katika hotuba yake kwa Bunge kuwa hatamvumilia mtu mzembe
na mvivu na kwamba watakaobainika kujihusisha na rushwa au ufisadi,
watashughulikiwa.
Ingawa wabunge karibu wote walikuwa wakimshangilia kwa nguvu wakati wa
hotuba yake hiyo, inadaiwa hamu ya kupata ulaji wa uwaziri inawafanya
baadhi yao kuingiwa na woga, kwani ufanyaji kazi wa mazoea ndiyo
unaowatesa.
“Nakuambia hapa wabunge, hasa wale wenye ndoto za kuteuliwa uwaziri wana
wasiwasi kama wataweza kweli kwenda na kasi ya huyu jamaa, maana
anaonekana kuwa siriaz sana na kazi. Hili liko wazi maana wengi walizoea
kuona nafasi za juu kiuongozi wanazitumia kwa masilahi yao,” kilisema
chanzo chetu katika viwanja vya Bunge mjini Dodoma.
Inadaiwa wengi wa wanaotegemea kupata uwaziri wana hofu kwa sababu
wanaamini mzigo watakaopewa utakuwa mkubwa kuliko tabia na hulka zao.
Rais Magufuli ameahidi kuteua Baraza dogo la Mawaziri litakalokuwa
limesheheni wachapakazi na katika kukabiliana na vitendo vya rushwa na
ufisadi, alisema kazi hiyo ataifanya kwa dhati.
Hata hivyo, mbali na jina la Tingatinga hivi sasa mtaani amepewa jina
jipya la Mtumbua majipu licha ya kuwa kitendo hicho huleta maumivu.
Tagged with: SIASA
Hakuna maoni :