Kamati Kuu ya CCM imefuta matokeo ya kura za maoni katika Jimbo la
Handeni, mkoani Tanga ambako Omar Abdallah Kigoda ambaye ni mtoto wa
mbunge wa zamani, marehemu Abdallah Kigoda alikuwa ameshinda.
Akizungumza jana, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye
alisema jana kuwa kutokana na kufutwa kwa matokeo hayo, uchaguzi wa kura
maoni katika jimbo hilo unarudiwa leo.
Alifafanua kuwa wagombea 11 waliwania nafasi hiyo lakini wawili kati
yao, Kigoda na Hamis Amad Mnondwa walipata kura zaidi kuwashinda wenzao.
Mkutano mkuu wa jimbo la Handeni, ulimchangua Omari Kigoda kwa kura 296
akiwashinda wenzake wawili Hamisi Mnondwa na Athumani Lukoya waliokuwa
wamechujwa kutoka miongoni mwa wanachama 11 walioomba nafasi hiyo.
“Lakini matokeo yanaonyesha hakuna mshindi aliyepata kura za kuridhisha
kuingia katika ushindani na vyama vingine, ndiyo maana Kamati Kuu
imeamua urudiwe,” alisema bila kutaja idadi ya kura walizopata wagombea
hao.
Mchakato huo wa kupata mgombea unafanyika kutokana na kifo cha aliyekuwa
mgombea ubunge wa jimbo hilo, Dk Abdallah Kigoda kilichotokea Oktoba
12, mwaka huu nchini India.
Nape alisema marudio hayo ya kura za maoni yatasimamiwa na makada watatu
wa CCM, Dk Maua Daftari, Dk Emmanuel Nchimbi na Abdallah Bulembo.
Nape alisema Kamati Kuu inaendelea na kikao chake cha siku moja ambacho
kina ajenda ambazo hakutaka kuzitaja. Kamati Kuu imefanya uamuzi huo
huku kukiwa na sintofahamu juu ya chama hicho kuanza ‘utaratibu mpya’ wa
kuwateua watoto wa vigogo wa chama hicho wanaofariki dunia wakiwa
wabunge au wagombea, kuwania nafasi iliyoachwa na wazazi wao.
Mbali na Omary, Goodluck Mtinga, mtoto wa aliyekuwa Waziri wa Nchi,
Ofisi ya Rais (Utumishi) Celina Kombani naye amepitishwa na chama hicho
kugombea ubunge katika jimbo la Ulanga.
Utaratibu kama huo ulitumika katika Jimbo la Kalenga mwaka 2014, CCM
ilipomsimamisha Godfrey Mgimwa, mtoto wa marehemu Dk William Mgimwa,
kugombea ubunge katika jimbo hilo lililokuwa likishikiliwa na baba yake.
Mwaka 2012, CCM pia ilimteua Sioyi Sumari kugombea ubunge katika Jimbo
la Arumeru Mashariki kuziba nafasi iliyoachwa na baba yake, marehemu
Jeremiah Sumari.
Hakuna maoni :