Aliyekuwa mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wa Chama cha
Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kupitia Umoja wa Katiba ya Wananchi
(Ukawa),
Edward Lowassa, amehoji maswali matatu kwa Rais Dk. John Magufuli.Katika
taarifa yake kwa vyombo vya habari jijini Dar es Salaam jana, Lowassa
amemtaka Rais Magufuli baada ya kusema hakuna mtoto atakayelipa ada
kuanzia Januari, mwakani, atamke mustakabali wa wanafunzi walioko
shuleni kama wataguswa na hatua hiyo au la.
Lowassa amesema kwa upande wake ahadi ya elimu bure aliyokuwa akiinadi
wakati wa kampeni, ilikuwa ni kuanzia shule ya awali hadi chuo kikuu na
kwamba hata wale walioko mashuleni, wangeguswa na hatua hiyo.
“Niliahidi watoto wote walioko na watakaoanza shule kuanzia kindergarten
(shule ya awali) hadi chuo kikuu, serikali yetu ingegharimia.
Na
nilitangaza kufuta michango yote shuleni ili kumpunguzia mzigo
mwananchi,” alisisitiza Lowassa ambaye amekataa kuyatambua matokeo ya
ushindi wa Dk. Magufuli akidai kuwa yeye ndiye aliyeshinda kwa asilimia
62 ya kura zote zilizopigwa.
Kuhusu suala la mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu, Lowassa amesema
yeye alishaweka wazi kuwa elimu ingekuwa bure hadi chuo kikuu.
“Vijana hawa wanahangaika na mikopo na nasikia ni asilimia 17 tu kati ya
wanafunzi 70,000 ndiyo waliopata mikopo. Sera ya Chadema na Ukawa kwa
ujumla, ni kufuta kabisa shida hizi kwa serikali kufadhili elimu yao,”
alifafanua Lowassa katika taarifa yake hiyo. Kwa msingi huo, Ukawa
kupitia kwa aliyekuwa mgombea wao wa urais, Lowassa, umewataka wananchi
kutofautisha ahadi ya elimu bure iliyotolewa na Rais Magufuli na ile
iliyotolewa na Ukawa.
Lowassa alisema Magufuli ametoa maelekezo kwa watendaji wa serikali
kuweka mikakati ya kutekeleza ahadi yake kuanzia Januari, mwakani kwamba
hakuna mtoto atakayelipa ada.
Hata hivyo, amesema hajaeleza waziwazi hatma ya wanafunzi walioko mashuleni kama wataguswa na hatua hiyo au la.
Hakuna maoni :