Ushiriki wa aliyekuwa Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Dk Tulia
Ackson katika masuala ya siasa na hatimaye kuchaguliwa Naibu Spika wa
Bunge, umezidi kuibua maswali huku akidaiwa kuwa amekiuka kanuni za
watumishi wa umma.
Wasomi, wanaharakati na wanasheria wameeleza kushangazwa na uteuzi huo,
kama ilivyokuwa Alhamisi alibobanwa kwa maswali bila majibu kuhusu ni
lini msomi huyo wa sheria alichukua kadi ya CCM na kuwania uspika na
baadaye unaibu spika kupitia chama hicho.
Hata hivyo, Dk Ackson amekanusha kukiuka kanuni za utumishi wa umma
akisema ile inayolalamikiwa kukiukwa (Kanuni za Utumishi wa Umma 2009),
ilifutwa kupitia waraka mpya uliotolewa na Katibu Mkuu Kiongozi Januari,
mwaka huu.
“Angalia hiyo ‘circular’ kifungu cha (5), kinasemaje, usiangalie hiyo
kanuni tena kwani imefutwa na huo waraka, ukisoma unaonyesha wazi. Zote
hizo unazoniambia nilizifahamu kabla ya kuchukua hatua yoyote,
sijakurupuka tu,” alisema.
Wiki iliyopita Dk Ackson akiwa mwanasheria wa Serikali alichukua fomu ya
kuwania uspika wa Bunge kinyume na matakwa ya kanuni za utumishi wa
umma, lakini baadaye alijitoa katika kinyang’anyiro hicho na kuwania
unaibu spika, baada ya kuteuliwa na Rais John Magufuli kuwa mbunge.
Mchakato wa Dk Ackson kuteuliwa kugombea hadi kushika nafasi hiyo umezua
maswali watu mbalimbali wakihoji ukiukaji wa kanuni hiyo inayozuia
wanasheria wa Serikali kujiunga na mambo ya siasa.
Akijibu maswali ya wabunge wakati akiomba kuchaguliwa kuwa naibu spika,
Dk Ackson alishindwa kueleza ni lini alichukua kadi ya CCM, hadi Spika
wa Bunge Job Ndugai alipoingilia kati akamruhusu kwenda kuketi.
Wachambuzi
Akizungumzia suala hilo, mwanaharakati kutoka HakiElimu, Godfrey
Bonaventure alisema kitendo cha Dk Ackson kuteuliwa kushika nafasi hiyo
kinaleta maswali mengi katika kanuni za utumishi wa umma na masuala ya
siasa.
“Miongozo iliyopo imeweka bayana kuwa wapo watumishi wa umma ambao
hawatakiwi kujihusisha na siasa kutokana na unyeti wa majukumu yao,”
alisema.
Alisema suala kubwa ambalo Dk Ackson anatakiwa kujibu kwa usahihi ni je, lini alianza kuwa mwanachama wa CCM?
“Watu wanaotakiwa kuhusika kwenye uamuzi mkubwa hawatakiwi kujihusisha
kwenye siasa. Hili suala lina mitego ambayo inavuruga mfumo wetu wa
uwajibikaji, inatupa shaka kwa sababu hawa watu maamuzi yao ni magumu,
uspika ni wajibu mkubwa,” alisema.
Bonaventure aliitaka Serikali kuheshimu miongozo yote ya utumishi wa umma ili vyombo hivyo viwe huru kufanya uamuzi.
“Alipoulizwa swali bungeni kuhusu lini alikuwa mwanachama wa CCM
hakuweza kutoa jibu sahihi, bila shaka angesema ni lini angeibua maswali
mengi zaidi,” alisema.
Alisema iwapo Dk Ackson angesema amekuwa mwana CCM kwa muda mrefu
angeibua maswali, lakini pia angesema amechukua kadi ya CCM hivi
karibuni angeibua hoja atawezaje kukifahamu chama na kujua namna ya
kuliongoza Bunge katika kipindi kifupi?
Mwanasheria wa kujitegemea, George Shayo alisema sheria inaweka wazi
kuwa watumishi wa Serikali hawatakiwi kushiriki katika siasa.
Makamu Mwenyekiti wa Chadema, Profesa Abdallah Safari alisema sheria zinakataza watumishi wa umma kujihusisha na siasa.
Profesa Safari ambaye pia ni wakili, alisema ingawa baadhi ya vipengele
vimefanyiwa marekebisho lakini wafanyakazi wa Mahakama na wanasheria wa
Serikali hawatakiwi kujihusisha na siasa.
“Ndiyo maana hata wakati Jaji Augustino Ramadhani alipochukua fomu ya
urais, tulimsema sana. Hata hizi sarakasi za Dk Ackson zinachekesha,
zinashangaza,” alisema.
Mhadhiri wa Sayansi ya Siasa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk
Alexander Makulilo alisema anafahamu kuwa kuna sheria kuhusu wafanyakazi
wa umma lakini haiwakatazi kujihusisha na siasa bali upo utaratibu wa
kufanya hivyo.
“Iko miongozo ya Serikali kuhusu watumishi wa umma lakini si kwamba
sheria inakataza, kwa mfano miongozo hiyo inawataka waache nafasi zao
pindi wanapotaka kuingia katika siasa,” alisema.
Home
/
SIASA
/
‘Mzimu’ wa Kanuni Wamwandama Naibu Spika..Wasomi Wadai Amekiuka Kanuni za Utumishi wa Umma
‘Mzimu’ wa Kanuni Wamwandama Naibu Spika..Wasomi Wadai Amekiuka Kanuni za Utumishi wa Umma
Tagged with: SIASA


Hakuna maoni :