TAARIFA YA JESHI LA POLISI KWA VYOMBO VYA HABARI
KUHUSU TAHADHARI KATIKA MKESHA WA MWAKA MPYA
Tunapoelekea kumaliza mwaka 2015 na kuukaribisha mwaka mpya wa 2016,
wananchi hutumia muda huo kwenda katika nyumba za ibada ama kusherekea
katika maeneo mbalimbali ya starehe, ambapo uzoefu unaonyesha kuwa
baadhi ya watu hupenda kutumia fursa hiyo kufanya vitendo
vinavyohatarisha usalama wa raia mali zao.
Jeshi la Polisi nchini, limejipanga vizuri katika mikoa yote kwa
kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama ili kuhakikisha
kwamba vitendo vyovyote vya uhalifu vitakavyojitokeza hususani katika
kipindi hiki cha kuelekea mkesha wa mwaka mpya vinadhibitiwa. Ulinzi
umeimarishwa kwenye maeneo yote ya kuabudia, fukwe za bahari, sehemu za
starehe na maeneo mengine yote ambayo yatakuwa na mikusanyiko mikubwa ya
watu.
Aidha, Jeshi la Polisi linatoa tahadhari kwa wananchi wote kuwa makini
na kuchukua hatua stahiki za haraka kwa kutoa taarifa pindi wanapoona
viashiria vyovyote vya uhalifu katika maeneo yao ya makazi ama maeneo ya
biashara. Simu za polisi endapo mwananchi atakuwa na taarifa ni 111 au
112.
Pia, Jeshi la Polisi linawatahadharisha wale wote ambao watakuwa
wakitumia barabara kuwa makini na kuzingatia sheria za usalama
barabarani na hasa kwa madereva wa magari na pikipiki, kuepuka kujaza
watu kupita kiasi, kwenda mwendo kasi, kutumia vilevi pamoja na kupiga
honi hovyo.
Vilevile, wananchi kuacha tabia ya kuchoma matairi barabani pamoja na
kupiga mafataki. Aidha, yeyote atakayefanya vitendo hivyo hatua kali za
kisheria zitachukuliwa dhidi yake.
Nawatakieni watanzania wote kheri ya mwaka mpya.
Imetolewa na:
Advera John Bulimba-SSP
Msemaji wa Jeshi la Polisi.
Makao Makuu ya Polisi.
Hakuna maoni :