UMESIKIA
mshambuliaji nyota wa TP Mazembe, Mbwana Samatta anaondoka zake kwenda
zake Nigeria kwa ajili ya shughuli ya utoaji wa tuzo za wachezaji bora
barani Afrika?
Tuzo
hizo zinafanyika Januari 7, mwakani. Samatta ataondoka Januari 5 na hali
halisi inaonyesha anaweza kuibuka na ushindi kwa kuwa ana nafasi.
Nafasi
yake inatokana na kazi kubwa aliyoifanya akiwa na TP Mazembe na
kuiwezesha kubeba ubingwa wa Afrika. Alifunga mabao katika mechi zote za
fainali, pia ameibuka kuwa mfungaji bora na kupata nafasi ya kucheza
Kombe la Dunia la Klabu nchini Japan.
Hiyo
ni safari ya kwanza ya Samatta, safari ya pili nayo inatarajia kuwa
mapema mwakani, anatarajiwa kwenda nchini Ubelgiji kujiunga na Klabu ya
Genk ya nchini humo.
Samatta
ameishamalizana na Genk kwa maana ya makubaliano, anachosubiri ni TP
Mazembe kumalizana Genk ili yeye amalizane pia na Wabelgiji hao
walioonyesha kweli wako makini walipoamua kuja hadi jijini Dar es Salaam
na kuzungumza na baba yake na familia yake kwa jumla, lakini wakamfuata
hadi Japan.
Samatta
ana safari mbili, kwanza tumuombee kwa Mwenyezi Mungu afanikiwe kwa
kuwa tayari ameonyesha ni mtu mwenye juhudi, anajitambua na amegeuka
kuwa alama ya taifa letu unapozungumzia soka huku akiwa ni mchezaji
aliyeibuka juzijuzi tu.
Wakati
Samatta anafunga safari hizo, nani amejipanga kuondoka naye? Nani
amejipanga angalau baadaye kusafiri safari kama hizo hapo baadaye? Au
ndiyo watu wanafurahia tu na kugeuza kinachofanyika ni kama filamu
ambayo baada ya picha yanafuatia majina ya waigizaji na wahusika
wengine?
Safari
ya Samatta haikuwa ya kuotea tu, alianza kwa hatua, alipambana, alikuwa
na malengo au ndoto na alitaka kuzitimiza. Hadi sasa bado hajatimiza
lakini akiwa njiani anapita katika barabara ya asali ambayo inamfanye
awe tofauti na wengi.
Samatta
amekuwa tofauti na wale waliokuwa mastaa, nyota wa miaka nenda rudi na
wengine sasa wamekuwa kama wendawazimu, siku zinavyokwenda wanadidimia
na vipaji vyao kwenda timu za chini au madaraja ya chini, “wanakufa na
vipaji vyao.”
Samatta
si malaika, si anayejua mpira kuliko Watanzania wote, lakini ukweli
nidhamu, kujituma na nia ya kufikia anachokitaka, vimembeba na
kubadilisha maisha yake. Tukubali huyu Samatta si yule wa Mbagala
Market, African Lyon wala Simba. Je, unakumbuka ni miaka mingapi
imepita? Tangu wakati huo nyota wangapi unawajua hadi leo wamesahaulika
kabisa?
Ndiyo
maana nikauliza hivi, nani anataka kuondoka na Samatta? Nikiwa
ninamaanisha hivi mwenye hamu ya mafanikio anayopata na mwenye kutaka
kuyafikia kwa kupambana kwa kuweka nia, kujituma na kujitambua.
Nani
anataka kubadilika? Kutoka wale mastaa wetu wa enzi zile au wa hivi
karibuni ambao maisha yao hadi leo hayako vizuri kwa kuwa wamekuwa watu
wa kubahatisha tu wakati walikuwa na vipaji lakini waliona Yanga na
Simba ndiyo mwisho wa reli!
Samatta
amefika alipo lakini haikuwa safari rahisi au laini. Hakika amepambana
na anayetaka kumfuata lakini akubali kupambana pia kufikia alipo na si
kulala na kutamani halafu akiamka tayari awe Samatta, itakuwa ni
kujidanganya.
Mafanikio
ya bila jasho ni yale ya haraka, yasiyojengwa na huporomoka haraka na
hayana muda mrefu. Wakati Samatta anaondoka, najua wengi sana mnatamani
au kumtamani angalau kufikia TP Mazembe na mafanikio aliyopata.
Basi
anzeni sasa, si kusubiri umri ukishawatupa mkono, ndiyo muanze
kukumbuka. Lazima mkubali kuumia, nidhamu pia iwabebe ili kufikia hapo
ili siku nyingine Mwenyezi Mungu akijaalia, nanyi muondoke kama yeye,
tuwasindike kwa pongezi na kiu ya kufikia mlichokifikia.
SOURCE: CHAMPIONI
Hakuna maoni :