Ukimya
wa wanasiasa walioongoza harakati za kupambana na ufisadi katika
majukwaa ya kisiasa, wakati huu Serikali ikichukua hatua za wazi na
haraka kukabiliana na ubadhirifu wa mali za umma, umeibua maswali kuhusu
uzalendo kwa nchi yao.
Miongoni
mwa wanasiasa waliohusishwa na maswali hayo ni pamoja na aliyekuwa
Waziri Mkuu, Frederick Sumaye, Mwenyekiti wa Taifa wa Chadema, Freeman
Mbowe na mgombea urais wa Chadema, Edward Lowassa.
Akizungumzia
sakata hilo jana, Mhadhiri Mwandamizi wa Masuala ya Siasa na Utawala wa
Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Benson Bana, alisema kama
kweli ni wazalendo, ni vyema wale wote waliokuwa wakipinga ufisadi
wajitokeze hadharani, kupongeza hatua zinazoendelea kuchukuliwa.
Profesa
Bana alisema hali inavyoendelea nchini kwa sasa ni wazi kwamba Rais
John Magufuli, anapaswa kuungwa mkono na wote waliokuwa wakipinga
ufisadi na ubadhirifu serikalini.
“Ni
wakati muafaka sasa wale wote waliokuwa wanapinga ufisadi wakiwemo
wanasiasa, wajitokeze hadharani kumuunga mkono Rais wetu, kama kweli
walisema hayo kwa uzalendo na uungwana,” alisisitiza Profesa Bana.
Alisema
ni wakati sasa wa Sumaye, Lowasa, Mbowe na wengine waliokuwa mstari wa
mbele kueleza umma ufisadi na ubadhirifu serikalini kwenye kampeni za
kuwania urais mwaka 2015, wakajitokeza hadharani kupongeza kazi
inayofanyika.
Pia
aliwataka wote waliosema hawataunga mkono serikali iliyoko madarakani,
kufuta mara moja kauli yao, kwani yanayoendelea kufanywa ni mambo mazuri
kwa ajili ya ustawi wa Watanzania wote bila kujali itikadi zao.
Magufuli na Ilani ya Ukawa
“Yapo
maneno kwamba Rais Magufuli anatekeleza ilani za vyama vingine na si ya
CCM, haya maneno yapuuzwe ni kukosa hoja, ilani za vyama vyote vya
siasa vinavyojitambua, zinajibu maswali haya ya wananchi,” alisema
Profesa Bana.
Akifafanua
hilo, Profesa Bana alisema kuna maneno yanaendelea kuzunguka kwa njia
ya ujumbe mfupi wa simu au kwenye mitandao ya kijamii, kuwa Dk Magufuli
anatekeleza ilani za vyama vingine vya siasa na kusisitiza hoja hiyo
haina mashiko.
Alisema
Dk Magufuli anatekeleza yale aliyoahidi kwenye kampeni alipokuwa
akiwania nafasi hiyo, kwa kuwa yapo kwenye Ilani ya CCM, huku
akisisitiza kuwa ilani za vyama vya siasa mwaka huu zilifanana kwa njia
moja au nyingine.
“Sisi
tulipata bahati ya kusoma na kuchambua ilani za vyama vitatu CCM,
Chadema na ACT-Wazalendo, tulipopitia ilani za vyama hivyo na vingine
vilivyoshiriki kwenye uchaguzi uliopita, tulibaini zote zinafanana,”
alisema Profesa Bana.
Alisema
kama kuna chama kinasema ilani inayotekelezwa ni yao, wangekuwa mstari
wa kwanza kujitokeza hadharani kumuunga mkono Rais Magufuli kwa
kutekeleza hayo, lakini kukaa kimya kunazua maswali mengi.
Wajuta kutompa kura
Alisema
ni vyema Rais apewe nafasi aendelee kutekeleza anayofanya kwa sababu
anajibu maswali ya wananchi yaliyokuwa yakisubiriwa kwa muda mrefu na
kwamba wapo baadhi ya wananchi wanajuta hivi leo kwa kutompigia kura.
“Tunazungumza
na watu mbalimbali wanatuambia wanajuta kumnyima kura Rais Magufuli,
kwa sababu kama asingeshinda, nchi ingekosa kiongozi mzuri na mwenye
kasi ya maendeleo kwa wote,” alisema Dk Bana.
Wapenda utajiri
Mhadhiri
mwingine wa chuo hicho, Profesa Kitila Mkumbo alitoa mwito kwa
Watanzania wote kumuunga mkono Rais Magufuli kwa kubadilisha mitazamo
yao ya kupenda vya bure, bali wafanye kazi kwa bidii.
Profesa
Mkumbo alisema juhudi zinazofanywa na Rais Magufuli, zitakuwa na tija
zaidi iwapo Watanzania wote watamuunga mkono kwa kubadilisha mitazamo
yao ya kupenda utajiri wa haraka haraka.
“Jitihada
za Rais Magufuli pekee hazitoshi, bali jamii yote ya Tanzania lazima
ibadilike, tuache kufanya vitu kwa mazoea na kupenda vya bure na utajiri
wa haraka haraka, bali tupende kufanya kazi kwa bidii,” alisema Profesa Mkumbo.
Alisema
masuala ya ubadhirifu na ufisadi ni mambo sugu yanayosumbua nchi na
hatua zilizoanzwa kuchukuliwa na Rais Magufuli ni nzuri kwani tofauti na
serikali zilizopita, yeye anatekeleza kwa kasi zaidi.
“Ubadhirifu
ni tatizo sugu nchini, lilianza kufanyiwa kazi tangu enzi za Mwalimu
Nyerere hadi Rais mstaafu Jakaya Kikwete, ila kwa awamu hii ya Rais
Magufuli, yeye anatekeleza kwa kasi zaidi,” alisema Profesa Mkumbo.
Home
/
SIASA
/
Ukimya wa Lowassa,Sumaye na Mbowe Kuhusu MAJIPU Yanayotumbuliwa na Magufuli Wazua Maswali
Ukimya wa Lowassa,Sumaye na Mbowe Kuhusu MAJIPU Yanayotumbuliwa na Magufuli Wazua Maswali
Tagged with: SIASA
Hakuna maoni :