IKIWA tayari Ubalozi wa Ubelgiji nchini Tanzania
umekwishatoa viza kwa mshambuliaji Mbwana Samatta kwenda kusaini klabu
ya KRC Genk, lakini taarifa zinasemekana kuwa huenda anaweza akabaki TP
Mazembe ya DRC kumalizia Mkataba wake hadi Aprili.
Hiyo inatokana na Rais wa Mazembe, Moise Katumbi kugoma
kumuuza Mwanasoka huyo Bora wa Afrika kwa wachezaji wa ndani katika
klabu hiyo Ligi Kuu ya Ubelgiji.
Rais wa Klabu ya TP Mazembe, Katumbi Moise.
Inasemekana pia kuwa, Katumbi anataka Samatta anende
kucheza Nantes FC ya Ligi Kuu ya Ufaransa, ambayo amekwishafikia
makubaliano nayo, na kwamba wiki iliyopita Nantes FC ilituma mwakilishi
wake jijini Dar es Salaam, ambaye alifanya mazungumzo na Meneja wa
Samatta, Jamal Kisongo mbele ya Ofisa mmoja wa Shirikisho la Soka
Tanzania (TFF).
Katika mazungumzo, Kisongo alifikia makubaliano ya maslahi
binafsi na Samatta ikiwemo dau la kusaini, mshahara, masharti na
marupurupu mengine. Kisongo alitaka kiwepo kipengele cha mchezaji
kutorejeshwa Afrika iwapo hatapata nafasi ya kucheza Nantes, bali auzwe
klabu nyingine ya Ulaya na ikakubaliwa.
Samatta
hivi karibuni akikabidhi jezi yake kwa rais Mstaafu, Dk Jakaya Kikwete
wakati Waziri wa Habari, Vijana, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Mh. Nape
Nnauye akishuhudia tukio hilo.
Nantes ilionesha nia ya dhati kabisa ya kumchukua Samatta
na Kisongo aliinuka kwenye meza ya mazungumzo akiwa amekubali na kusema
anakwenda kuzungumza na mchezaji. Hata hivyo, inaonekana Samatta
mwenyewe ndiye anayetaka kwenda Ubelgiji na si Ufaransa, kwani kitendo
cha Kisongo kutorejesha majibu kwa Nantes kinaashiria ameshindwa
kumshawishi mchezaji wake akubali ofa hiyo.
Wakati huo huo, Rais wa Mazembe hayuko tayari kumuuza
Samatta Ubelgiji na yuko tayari kuona Samatta anabaki Mazembe kumalizia
Mkataba wake ili aondoke kama mchezaji huru Aprili, hali ambayo
itamlazimu kusubiri hadi Agosti kusaini Genk.
Kwa sasa, kambi ya Samatta inajaribu kuomba msaada kwa
viongozi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wakazungumze na
Katumbi ili akubali kumuacha mchezaji aende klabu aliyochagua.
Rais Mstaafu, Dk Jakaya Mrisho Kikwete ambaye kwa sasa ni
Mwenyekiti wa chama tawala, CCM, Waziri wa Michezo, Nape Nnauye kwa
pamoja wameahidi kumsaidia Samatta katika suala la kumlainisha Katumbi
akubali kupokea ofa ya Genk.
Wakati huo huo, Nantes wamekuwa wakimpigia simu Kisongo
wakisema wanamsubiri mchezaji aende kusaini, lakini Meneja huyo anakosa
majibu ya uhakika.
Inaonekana tayari Katumbi anaujua mchezo wote unaoendelea
naye ameamua kukaa kimya akiamini Samatta hawezi kufanya chochote kwa
sasa bila baraka zake. Wazo la kusema Samatta asubiri hadi mwezi Aprili
atakapomaliza Mkataba wake ili kusaini kama mchezaji huru mwezi Agosti,
halifurahiwi hata na Kisongo mwenyewe.
Samatta aliyejiunga na TPM mwaka 2011 akitokea Simba SC
aliyoichezea kwa nusu msimu, akitokea African Lyon, hadi sasa ameichezea
klabu hiyo mechi 103 na kuifungia mabao 60. Ndani ya mechi hizo, kijana
huyo wa umri wa miaka 24, ameshinda taji la Ligi ya Mabingwa Afrika na
Mazembe, huku naye akiibuka mfungaji bora wa michuano hiyo na kutwaa
tuzo ya Mchezaji Bora Anayecheza Afrika.
Hakuna maoni :