MKATAJI vichwa vya raia kutoka mataifa ya magharibi katika kundi la
kigaidi la Dola ya Kiislam (IS), Mohammed Emwazi, ametangazwa kuuawa.
Emwazi anatambuliwa zaidi kwa jina la Jihadi John, ndiye aliyekuwa
akitumiwa zaidi kwenye video ambazo zilikuwa zikioneshwa na kundi hilo
wakati wa kutekeleza mauaji ya raia wa mataifa ya magharibi walilokuwa
wakikamatwa na kundi hilo.
Raia huyo wa Uingereza alikuwa akitafutwa kwa udi na uvumba na wanajeshi
wa mataifa ya magharibi kutokana na kuhusika zaidi katika kutesa na
kuua raia wa mataifa hayo walikokamatwa na kundi hilo.
IS wametangaza kifo cha Emwazi katika jarida lao la mtandaoni
lijulikanalo kwa jina la Dabiq. Taarifa ya IS inaeleza kuwa mwanamgambo
huyo aliuawa kwenye shambulio lililotekelezwa na ndege zisizokuwa na
rubani Novemba mwaka jana.
Hata hivyo, Marekani baada ya kufanya shambulio lake dhidi ya Emwazi
mwaka jana mjini Raqqa, ilieleza kutokuwa na uhakika wa kumuua
mwanamgambo huyo.
Emwazi alionekana mara kwa mara kwenye video za kikatili za kundi hilo,
miongoni mwayo ni ile iliyoonesha akiwakata shingo mateka kutoka mataifa
ya magharibi wakiwemo Muingereza David Haines ambaye alikuwa mfanyakazi
wa shirika la kutoa misaada na Alan Henning ambaye alikuwa dereva wa
teksi.
Lakini IS kwenye tangazo lao walimtaja Emwazi kwa jina la Abu Muharib
al-Muhajir kutokana na kupenda kulitumia ndani ya kundi hilo wakati wa
uhai wake.
IS wanaeleza kuwa Emwazi alifariki dunia Novemba 12 kwenye gari lililoshambuliwa na ndege zisizo na rubani katika mji wa Raqqa.
Waliweka picha ya Emwazi akionekana kutabasamu. Alizaliwa Kuwait mwaka 1988 na kuhamia Uingereza mwaka 1994.
Hakuna maoni :