NAHODHA wa Timu ya Taifa ya Brazil ambae pia huchezea Klabu ya Spain Barcelona, Neymar, ameshitakiwa huko kwao Brazil kwa ukwepaji kodi na kugushi makabrasha kwa kipindi cha Miaka 7.
Ofisi za Mwendesha Mashitaka huko Brazil zimedai uhalifu huo umetendeka kuanzia 2006, wakati huo Neymar akichipukia Soka na kuichezea Klabu ya Brazil Santos, hadi 2013 alipohamia Barcelona.
Pamoja na Neymar, wengine waliounganishwa kwenye Kesi hii ni Baba yake Mzazi na Rais wa sasa wa Barcelona, Josep Maria Bartomeu, pamoja na Rais alietangulia wa Klabu hiyo, Sandro Rosell.
Klabu ya Barcelona inayo Kesi nyingine huko Spain ambapo Kampuni ya Uwekezaji ya Brazil, DIS, imedai kudhulumiwa kuhusiana na Uhamisho wa Neymar kutoka Santos kwenda Barcelona Mwaka 2013.
Katika Kesi hiyo, Neymar, ambae si Mshitakiwa, alitoa ushahidi kwenye Mahakama Nchini Spain Jumanne iliyopita.
Mwenyewe Neymar, Siku zote amekuwa akikanusha kuhusika na njama zozote.
DIS ilikuwa ikishikilia Asilimia 40 ya thamani ya Kibiashara ya Neymar wakati alipokuwa akiichezea Santos na imedai kudhulumiwa wakati wa Uhamisho wa Neymar kutoka Santos kwenda Barcelona.
Awali, Barcelona ilitangaza Uhamisho wa Neymar uligharimu Euro Milioni 57.1 lakini Mamlaka za Mahakama za huko Spain zinakisia Uhamisho huo ulikuwa na thamani isiyopungua Euro Milioni 83.3 huku tofauti yake ikiingia mifukoni mwa Neymar na Familia yake pamoja na Klabu ya Santos.
Neymay, pamoja na Lionel Messi na Luis Suarez, ndio Mastaa wakubwa kwenye Timu ya Barcelona.
Lakini Klabu hiyo imekuwa ikikumbwa na Kesi kadhaa zikihusu ukwepaji Kodi Wachezaji wake kama vile Mascherano na Messi ambae atasimama kizimbani Mei 31 kujibu tuhuma za ukwepaji Kodi.
Hakuna maoni :