Siku
za wauza unga sasa zinahesabika baada ya Tume ya Kudhibiti Dawa za
Kulevya kuvunjwa rasmi na chombo kingine kitakachokuwa na mamlaka ya
kuchunguza, kukamata, kupekua, kuteketeza na kuwapeleka mahakama
kikitarajiwa kuundwa hivi karibuni.
Hatua
hiyo imekuja baada ya Sheria ya Dawa za Kulevya ya mwaka 1995 kufikia
kikomo Septemba 14 na kutungwa kwa sheria mpya ya kupambana na dawa za
kulevya ya mwaka 2015 iliyoanza kutumika Septemba 15, mwaka huu.
Machi
mwaka huu, aliyekuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu
na Bunge), Jenista Mhagama wakati akisoma muswada wa Sheria ya
kudhibiti na kupambana na dawa za kulevya (the drug control and
enforcement act, 2014) bungeni Dodoma, alisema Serikali inakusudia
kuanzisha chombo kinachojitegemea chenye mamlaka ya kiutendaji ya
kuchunguza, kupekua na kukamata watuhumiwa tofauti na ilivyokuwa tume
ambayo haikuwa na mamlaka ya kudhibiti na kupambana na tatizo hilo.
Katika
mapambano hayo dhidi ya dawa za kulevya tofauti na sheria inayotumika
sasa, chombo hicho kitajikita katika maeneo muhimu ikiwamo; kudhibiti
mbegu za mimea ya dawa za kulevya, kuongeza viwango vya faini na
nyongeza ya kifungo badala ya kuwa mbadala wa kifungo, na kutoa adhabu
kutokana na uzito wa kosa.
Mapendekezo
yaliyotolewa na kwa mujibu wa Muswada huo, watakaobainika kufanya
biashara ya dawa za kulevya watozwe faini ya Sh1 bilioni moja au kifungo
kisichopungua miaka 30 jela.
Pia,
atakayekutwa analima, kusambaza mbegu, kusafirisha, kuzalisha au
kuingiza mimea inayozalisha dawa za kulevya kama bangi, mirungi na
cocaine atatozwa faini isiyopungua Sh 20milioni, kifungo kisichozidi
miaka 30 au vyote pamoja.
Akiwa
kwenye mikutano ya kampeni, Rais John Magufuli alitangaza mapambano
dhidi ya dawa za kulevya na alipozindua Bunge Novemba 20, aliwaomba
Watanzania wamuombee katika mapambano hayo aliyoyasema kuwa ni magumu.
Wakati
akihutubia Bunge mjini Dodoma, Rais Magufuli alisema dawa za kulevya ni
janga kwa taifa na kundi linaloathirika zaidi ni vijana wa kiume na
kike.
Aliongeza kusema kuwa familia nyingi zimeathirika na nguvu kazi ya taifa imepotea kutokana na matumizi ya dawa hizo za kulevya.
“Tutaushughulikia mtandao huo hususan wafanyabiashara wakubwa wanaojihusisha na dawa za kulevya bila ajizi,” alisema.
Hata hivyo, hadi sasa uundwaji wa chombo kipya haujakamilika hadi Rais atakapomteua kamishna wa kukiongoza.
Msemaji
wa tume hiyo, Florence Mlay, alisema tume ipo katika hatua za
mabadiliko kuelekea kuwa chombo kamili kutokana na sheria mpya ya mwaka
2015.
“Hiki chombo kitakuwa na mabadiliko na kitakuwa na majukumu makubwa zaidi tofauti na ilivyokuwa tume,” alisema.
Katika
miaka ya 90, Serikali ilianzisha vitengo vya kudhibiti dawa za kulevya
katika baadhi ya idara na taasisi zake ili kuimarisha jitihada za
udhibiti wa dawa za kulevya nchini.
Taasisi
hizo ni Jeshi la Polisi, Idara ya Usalama wa Taifa na Idara ya Ushuru
wa Forodha. Pamoja na jitihada hizo, tatizo la dawa za kulevya
limeendelea kukua, mwaka 1995, Bunge lilitunga Sheria ya Kuzuia Biashara
Haramu ya Dawa za Kulevya Namba 9 ya Mwaka 1995 (Sura 95).
Sheria
hiyo ilianzisha Tume ya Kuratibu Udhibiti wa Dawa za Kulevya ambayo
ilianza kazi mwaka 1997, chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu na mwenyekiti wa
Tume ni Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Akizungumzia
sheria mpya ya dawa za kulevya, Mkuu wa Kitengo cha Kupambana na Dawa
za Kulevya nchini, Alfred Nzowa alisema katika sheria mpya, dawa za
kulevya hazihifadhiwa kama ilivyo sasa bali zitaharibiwa baada ya kupata
hati ya uthibitisho kutoka kwa Mkemia Mkuu wa Serikali.
“Tume
haipo tena hii ni baada ya kuundwa kwa sheria mpya, lakini chombo kipya
kitakachoundwa kitakuwa na meno zaidi ya tume na kitakuwa na vitengo
hadi mikoani,” alisema.
Alisema
sheria hiyo mpya ya dawa za kulevya haijaathiri kitengo cha kupambana
na dawa za kulevya kwa kuwa kimeundwa na Inspekta Jenerali wa Polisi
(IGP).
Kesi 105 za dawa za kulevya
Akizungumzia
kesi za dawa za kulevya nchini, Kamanda Nzowa alisema mpaka sasa bado
kesi 105 zipo katika hatua ya kusikilizwa na watuhumiwa wengine
wamehukumiwa.
Nzowa
alitoa mfano wa Anna Mboya kuwa alikamatwa Novemba 2, 2011 na gramu
1,140 za dawa za kulevya aina ya cocaine na kuhukumiwa kwenda jela miaka
20 na kutozwa faini ya Sh 148.1 milioni.
Kesi
nyingine ni ya raia wa Nigeria Chukwudi Okechukwu na wenzake watatu,
Paul Ikechukwa Obi, Shoaib Muhammad Ayaz na Hycenth Stan ambao
walihukumiwa jela miaka 30 kila mmoja na kulipa faini ya Sh9 bilioni.
Chukwudi na wenzake walibeba kilo 81 za dawa za kulevya aina ya heroine.
Mtuhumiwa
mwingine aliyehukumiwa hivi karibuni alitambulika kwa jina moja la
Fred, alikamatwa na kilo 180 za heroine maeneo ya Mbezi Jogoo na
kuhukumiwa jela miaka 20 na kulipa faini ya Sh15 bilioni.
Kamanda
Nzowa alisema kukamatwa kwa watuhumiwa wa dawa za kulevya hakuna ujuzi
bali ni taarifa zinazoletwa na wasamaria wema ndizo zinazosaidia.
“Mashine
ya X-ray peke yake haisaidii chochote, lakini taarifa zinazotusaidia ni
zile zinazoletwa na raia wema halafu sisi tunazithibitisha kwa mashine
maalum ya poligrahic,” alisema.
Alisema mashine hiyo inawasaidia kugundua mtu kasema uongo au ukweli pindi anapopeleka taarifa katika kitengo hicho.
“Wasamaria
wema wakituambia, sisi tunaanza kazi mara moja, tunahakikisha kama
taarifa ni za kweli kwa kutumia mashine hiyo, inatueleza kama mtu
anasema kweli,” alisema.
Hakuna maoni :